February 26, 2024
Majanga yalipiga eneo lenye milima la Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara, Tanzania, mnamo Desemba 2023, baada ya mvua kubwa kusababisha maporomoko ya udongo na mafuriko ambayo yalipeleka mawe na magogo katika vijiji, kuvunja nyumba, kuua watu na kuwahamisha wengine.
Kijiji cha Gendabi, ambacho hapo awali kilikuwa uwanja wenye shangwe uliopambwa na kicheko cha watoto, kilipata athari mbaya za asili.
"Watoto walikuwa wanacheza hapa, wakati wa mapumziko ya darasani au baada ya shule." Mkaazi wa kijiji cha Gendabi, kimoja kati ya vijiji vinne vilivyokumbwa zaidi na mafuriko.
Majanga hayo yaliharibu mazao, kuuwa mifugo, na kuvuruga huduma za afya, elimu, na miundombinu, ikiwa ni pamoja na barabara, vyanzo vya maji, umeme, na mifumo ya mawasiliano.
Kulingana na Idara ya Usimamizi wa Majanga ya Tanzania, angalau watu 89 waliopoteza maisha yao ikiwa ni pamoja na watoto, na takriban watu 5,600 walikumbwa na mafuriko na maporomoko ya udongo. Miongoni mwao, zaidi ya watu 700, ikiwa ni pamoja na watoto, walilazimika kuhama makazi yao na kuhifadhiwa katika shule tatu za msingi.
"Vitabu vyangu vyote vya mazoezi na sare za shule vimepotea," alisema Joseph mmoja wa watoto waliohamishwa makazi yao kutokana na mafuriko. Kabla ya janga kutokea, alikuwa anajiandaa kuanza Darasa la 7. "Sijui, nitapataje tena fursa ya kwenda shule," alisema akiashiria wasiwasi na changamoto sawa zinazokabiliwa na watoto wengi baada ya janga.
Chini ya uongozi wa Serikali ya Tanzania, UNICEF na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa walichukua hatua haraka kutoa msaada kwa jamii zilizoathiriwa.
"Tulisambaza vifaa vya msaada, ikiwa ni pamoja na maji safi na huduma za usafi, tulitoa huduma za usafi ambazo ni muhimu katika kuzuia magonjwa kama Kipindupindu katika makambi yenye msongamano. UNICEF pia iliwatuma maafisa wa ustawi wa kijamii kutoa msaada wa afya ya akili na ushauri wa kisaikolojia, hasa kwa watoto walio hatarini kwa unyanyasaji na ukatili." Stanislaus Kamwaga, Mtaalam wa UNICEF katika Masuala ya Maji, Usafi, na Afya (WASH).
Serikali ya Tanzania inafanya jitihada za kuhamisha familia na kuunganisha tena wazazi na watoto waliohamishwa makazi yao.
Shule ambazo hapo awali zilitumika kama makambi zinatarajiwa kufunguliwa tena, zikipatia nafasi wanafunzi kama Joseph, ambao wanatafuta fursa ya kurudi darasani licha ya janga lililowaathiri katika kijiji chao.